





VIGOGO wawili katika sakata la kutaka kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kutoka nchini Indonesia, Andrew Chan na Myuran Sukumaran wanatarajia kuuawa kwa kupigwa risasi kesho Jumatano asubuhi.
Familia za vigogo hao jana zilitawaliwa na simanzi wakati zikiwaaga kwa mara ya mwisho wapendwa wao hao waliopo katika gereza moja kwenye Kisiwa cha Nusakambangan nchini Indonesia.
Majeneza ya Chan na Sukumaran tayari yamepelekwa katika kisiwa hicho kinachojulikana kwa jina maarufu la 'death island' likimaanisha kisiwa cha kifo.
Andrew Chan na Myuran Sukumaran walikuwa viongozi wa kundi la watu tisa walionaswa wakitaka kusafirisha kilo 8.3 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya bilioni 6, Aprili 17, 2005 huko Denpasar, Bali nchini Indonesia. Kundi hilo lilipewa jina la Bali Nine.
Kundi la Bali Nine lilikuwa likiwahusisha raia wa Australia tisa ambao ni Andrew Chan, Si Yi Chen, Michael Czugaj, Renae Lawrence, Tan Duc Thanh Nguyen, Matthew Norman, Scott Rush, Martin Stephens na Myuran Sukumaran.
Mwaka 2006 watuhumiwa saba kati ya tisa walihukumiwa kifungo cha maisha jela huku Andrew Chan na Myuran Sukumaran wakihukumiwa kuuwa kwa kupigwa risasi.