Benki ya NMB jana January 26 imekabidhi hundi ya shilingi Milioni 75 kama udhamini wa mkutano wa mwaka wa maafisa wa Polisi nchini unaendelea Dodoma katika ukumbi wa Kimataifa wa St. Gasper.
Mkutano huo unajumuisha makamishna, makamanda wa mikoa ya Tanzania bara na visiwani pamoja na maafisa wakuu waandamizi wa Jeshi hilo kutoka Makao makuu.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Tom Borgols amesema udhamini huo unajumuisha usafiri wa mabasi kwa washiriki wote kutoka mikoa yote ya Tanzania bara na visiwani, pamoja na maandalizi ya mkutano huo.
“Jeshi la polisi ni wadau wetu muhimu ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa muda mrefu, sisi kama NMB tumefarijika sana kudhamini mkutano huu kwani kutoka katika mkutano huu, mipango na mikakati itakayojadiriwa itakuwa ni manufaa makubwa kwa nchi yetu pamoja na benki ya NMB ambayo matawi yake yote Zaidi ya 170 nchini kote yanapatiwa ulinzi kutoka jeshi la polisi.”– Tom Borgols.
Mbali na udhamini huo, NMB imewela mabanda kadhaa ya maonyesho katika eneo la Ukumbi huo ambapo wanatoa huduma mbalimbali kama kutoa na kuweka fedha kupitia huduma ya NMB Wakala; huduma mpya inayoshirikisha mawakala wa Max Malipo, kufungua akaunti kupitia Chap Chap Instant Account pamoja na kutoa elimu juu ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo.
Mkutano huo utadumu kwa muda wa siku 5, umeanza Jumatatu January 26 mpaka Ijumaa tarehe 30.