Thursday, January 22, 2015

WEMA AMFUNGULIA KESI DIAMOND POLISI

MKALI wa filamu nchini na Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu ‘Wema’, amemfungulia kesi ya madai mpenzi wake wa zamani ambaye ni mwanamuziki wa bongo fleva, Nassib Abdul ‘Diamond’, kwa kumtapeli kiasi cha Sh milioni 10.
Kwa mujibu wa mtandao wa Shirika la Utangazaji (BBC) idhaa ya Kiswahili, Wema aliripoti madai yake kituo cha Polisi Oysterbay akidai kuwa alimpatia mwanamuziki huyo kiasi hicho kwa makubaliano ya kazi na kuahidi kumlipa, lakini amekwenda kinyume makubaliano yao.
Muhusika mkuu ambaye ni Wema alitoa maelezo kwamba watu wanamtupia lawama kutokana na hatua aliyofikia, lakini amedai kuwa amelazimika kufanya hivyo kwa kuwa yeye ndiye aliyeingia dhamana na taasisi Focus Vicoba kuchukua fedha hizo.
“Naona watu wengi wananilaumu kwa kuwa nimemfungulia kesi Diamond, pasipo kuelewa kama fedha hizo pia hazikua zangu bali ni mkopo ambao niliingia dhamana katika taasisi ya utoaji mikopo ya Vicoba.
“Kupitia mfuko wa Focus Vicoba nilichukua mkopo huo kwa lengo la kumpatia Diamond, ili aweze kuandaa miradi yake tena kwa makubaliano kuwa atazirudisha ili tuweze kufanya marejesho ya mkopo tuliochukua,” alisema Wema.
Mrembo huyo alieleza muda waliiopeana ahadi ya kurudisha fedha hizo umepita na Diamond haoneshi dalili ya kuzirejesha wakati wanatakiwa kuzirudisha kwa wakati .
“Yote haya yasingenikuta, lakini sina jinsi kwani natakiwa kurudisha pesa za watu nimekuwa nikimpigia simu Diamond hataki kupokea simu zangu, lakini kama alitaka kunidhulumu ni bora angejiunga mwenyewe na hawa Vicoba ili apate mkopo na kufanya mambo yake au kama aliona hawezi kwa kujishtukia basi angetumia ile tovuti yao, angepata kwa urahisi na hakuna mtu yeyote angejua kama amekopa ila sio kukimbia kulipa deni la watu,” alisema.
Hata hivyo Diamond ambae kwa sasa yupo nchini Burundi kwa ajili ya ziara yake kimuziki, tayari ametumiwa taarifa na jeshi la polisi kwa barua ya wito kufika kituoni pindi atakaporejea nchini, huku mama yake mzazi akifikishiwa ujumbe huo nyumbani kwake.
Wema ambae alimwekea dhamana, yupo katika kipindi kigumu ambacho kinaweza kupelekea kufilisiwa mali zake ambazo aliziandikisha wakati wa kuchukua mkopo huo ili ziweze kufidia deni hilo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa taasisi hiyo ambae aligoma kutajwa jina lake gazetini, alisema kuwa ni kweli Wema alifika katika ofisi zao zilizopo Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, ili apewe muongozo lakini alipotakiwa kufuata taratibu za kiofisi kama wanachama wengine wanavyofanya katika vikundi, hakukubaliana na utaratibu, hivyo kushauriwa ajiunge kupitia tovuti .
MTANZANIA ilimtafuta Meneja wa Wema, Martin Kadinda, ambae alieleza hajui chochote kuhusu kufungulia kwa kesi hiyo, akaomba apewe muda kumtafuta msanii huyo ili aweze kupata ufafanuzi juu ya suala hilo, lakini hakueleza nini kilichojiri na kusisitiza asubiriwe.
Gazeti hili halikuishia hapo, lilimsaka Meneja wa Diamond, Babu Tale, ambae alionekana kushtushwa na habari hizo na kudai kuwa hazina ukweli wowote.
Source: Mtanzania Web

Comments System

facebook

Disqus Shortname

Powered by Blogger.