Monday, September 5, 2016

Eneo la Kariakoo,Dar es salaam lapewa hadhi ya Mkoa na TRA.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imelipa hadhi ya mkoa maalum eneo la  Kariakoo  Dar es Salaam kutokana na eneo hilo kuwa  kitovu cha biashara nchini.
 Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hayo alipokua akitoa takwimu za mapato kwa mwezi August,2016 na kudai kuwa TRA iimevuka lengo kwa kukusanya   Sh trilioni 1.158 tofauti na lengo lao la kukusanya  trilioni 1.152 ambayo ni   asilimia 100.57.

Aidha ameongeza kuwa makusanyo hayo yametokana na matunda mazuri ya mikakati iliyowekwa  mamlaka hiyo na kuongeza kuwa makusanyo hayo yamevuka lengo ikilinganishwa na yale ya   Agosti 2015 ambapo zilikusanywa  Sh bilioni 923.
                                                  Richard Kayombo.

“Sambamba na hayo pia tunaomba wananchi na wafanyabiashara kuendelea kujitokeza kuhakiki taarifa zao za usajili wa namba za utambulisho kabla ya Oktoba 15 mwaka huu katika vituo husika. Baada ya muda huo kuisha hautaongezwa muda na badala yake hatua hiyo itahamishiwa katika mikoa mingine,” alisema Kayombo.

Kayombo pia amewataka wafanyabiashara wa vituo vya mafuta wawe wamefunga mashine za EFDs ifikapo Septemba 30, mwaka huu  na kwamba Oktoba mosi TRA itaanza hatua ya ukaguzi kwenye vituo vyote vya mafuta nchini na  vituo vitakavyokuwa vimekaidi agizo hilo hatua za kisheria  zichukuliwa huku  akiwasihi walipa kodi wote waliosajiliwa na VAT wanatakiwa kuwasilisha mrejesho wa  hesabu ya biashara zao ya kila mwezi ifikapo tarehe 20 ya kila mwezi badala ya 27 iliyokuwa ikitumika mwaka wa fedha uliopita.

William Herzon-Mtanzania.

Comments System

facebook

Disqus Shortname

Powered by Blogger.