Mtandao wa kijamii wa Facebook umenunua programu ya huduma za
meseji ya WhatsApp kwa dola za marekani bilioni 19 (TSh 30.9 trilioni)
katika taarifa iliyotoka mapema leo.
Ununuzi huo wa WhatsApp umetengeneza mabilionea
wapya angalau watatu, akiwemo mwanzilishi wa WhatsApp, Jan Koum, ambaye
atajiunga na bodi ya wakurugenzi ya Facebook.
Mwanzilishi mwenza wa WhatsApp, Brian Acton, naye anaingia katika orodha ya mabilionea wapya vijana.
Miaka 4 iliyopita, Acton alijaribu kuomba kazi
Facebook na Twitter baada ya kupunguzwa kutoka Yahoo, inaripoti blogu ya
teknolojia ya Techcrunch.
Hakufanikiwa.
Leo hii, program aliyoitengeneza na rafikiye wa
Yahoo, Koum, inagombaniwa na kampuni zilezile zilizomkataa na hatimaye,
imenunuliwa kwa mabilioni ya dola na Facebook.
Wengine walioula ni wawekezaji wa kwanza wa WhatsApp toka kampuni ya uwekezaji ya Sequoia.
Techcruch inaripoti vijana wa Sequoia
wametengeneza zaidi ya dola bilioni 3 (TSh 4.9 trilioni) – mara 50 ya
pesa waliowekeza – katika ‘dili’ hilo.
Facebook, ambao ni mtandao mkubwa kuliko yote
duniani ukiwa na wanachama zaidi ya bilioni 1, inaamini kuwa WhatsApp
itasaidia kuongeza uwepo wake katika masoko mbalimbali duniani, hasa
katika nchi zinazoendelea Afrika, Asia na Amerika Kusini ambapo
teknolojia ya simu za mkononi imeshika hatamu.
Uamuzi huo unaipa Facebook nafasi ya kuongeza
idadi ya watumiaji wa mtandao wake, itarithi zaidi ya watumiaji milioni
450 wa WhatsApp.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook,
Mark Zuckerberg anaamini uamuzi wa kuinunua WhatsApp kwa dola bilioni 19
ni wa busara, kwa kuwa “[WhatsApp] ni mtandao unaokuwa kwa haraka,
ambayo itafikia watumiaji zaidi ya bilioni moja hivi punde.”