Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mnamo tarehe 10 Desemba 2016, alikutana na kufanya mazungumzo na Mmiliki wa
Kiwanda cha Saruji cha 'Dangote' kilichopo mkoani Mtwara,kinachomilikiwa na Mfanyabiashara Bilionea raia wa Nigeria, Alhaji Aliko Dangote.
Katika mazungumzo hayo, Rais Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara huyo
kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa
wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya
Viwanda.
Rais Magufuli amesema kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote
kilichopo Mkoani Mtwara hapakuwa na tatizo lolote ila kulikuwa na watu
ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya
biashara za ujanja kitu ambacho serikali yake haikiruhusu.
Amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka Shirika la Mafuta na Gesi nchini (TPDC) ambacho ni
chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya
kutengeneza faida tu.
''Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na
viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili
ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili ''
amesema Rais Magufuli.
Dokta Magufuli amesema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia
kusafirishia saruji yake wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa
shilingi bilioni 43 kitu ambacho hakina uhalisia wowote bali ni watu
ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.
Kwa upande wake mmiliki wa Kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote,
Alhaji Aliko Dangote ameshangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa
amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya
Tanzania kitu ambacho amesema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya
mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.
Katika kuthibitisha hilo, tayari Mfanyabiashara huyo ameingiza malori
mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake. Ameongeza kuwa lengo la
kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia ana lengo la
kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya
kuagiza mali ghafi toka nje ya nchi ambazo zinapatikana nchini.
Alhaji Dangote amemuhakikishia Rais magufuli kuwa ataendelea kufanya
kazi na Serikali ya Tanzania na kamwe hana nia yoyote ya kufunga kiwanda
chake kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari bali ana mpango
wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa nchini kutokana na
uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Katika hatua nyingine Rais Dkt. John Pombe Magufuli amuapisha Mkuu wa
Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Olonyokie Ole-Sendeka anayechukua nafasi
ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu
wa Mkoa wa Singida.
Wengine walioapishwa na Rais Magufuli ni Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye
anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo (Kilimo), Dkt.
Maria Sasabo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
(Mawasiliano), Dkt. Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii na Bibi Grace Alfred Martin kuwa Balozi (Mkuu wa
Itifaki).
Jaffar Haniu,
Naibu Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, IKULU.
Dar es Salaam.
10 Desemba, 2016.