WAKATI mastaa kadhaa wa kike wa filamu Tanzania
wakionekana umri wao kuwatupa mkono, lakini wakiwa hawana ndoa wala
watoto, baadhi yao wamefunguka kuwa wanahitaji zaidi kupata uzao kuliko
kuishi maisha ya kuolewa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam, walisema suala
la ndoa ni majaaliwa na si jambo unaloweza kupanga, kwa vile mwenye
uwezo wa kufanya hayo yote ni Mungu, kama ilivyo katika kuamua kuzaa au
la.
Coletha Raymond ‘Koletha’, alisema katika maisha ya Kitanzania,
wanaume ndiyo wenye uwezo wa kuamua. wataoa lini na ikawa kwa sababu wao
ndiyo wanaotongoza, lakini mwanamke hawezi kusema.
“Kuolewa natamani sana lakini bado sijapata mwanaume sahihi, naendelea
kumuomba Mungu anipe, nawaomba na wengine wanisaidie kuomba, kuhusu
kuzaa niko tayari hata kama sijaolewa,” alisema.
Kauli kama hiyo ilitolewa pia na msanii wa filamu Lulu Semagongo
‘Anti Lulu’ aliyesema yupo tayari kuzaa hata kabla ya ndoa kwa sababu
kuitwa mama kwake ni muhimu kuliko ndoa.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Baby Madaha ambaye pia anafanya
muziki, alisema hana anachotamani kati ya ndoa wala mtoto, isipokuwa
kitu muhimu kwake kwa sasa ni pesa.
“Katika maisha yangu sina mpango wa kuolewa wala kuzaa,
ninachotafuta zaidi ni pesa na umaarufu, dunia nzima initambue, sijali
cha umri wala nini, hayo ndiyo maamuzi ya maisha yangu.”
“Mimi siwezi kujua nitaolewa lini kwa sababu Mungu ndiye anajua ubavu
wangu uko wapi na anakuja kwangu lini, pia siwezi kuwa na uhakika kama
niliyenaye ndiyo ubavu wangu.
“Naweza nikasema naolewa mwaka huu kumbe nikaja kuolewa miaka miwili
mbele. Suala la kuzaa kiukweli hakuna kitu natamani sasa hivi kama
mtoto, hili sizungumzii sana, litakuwa ni sapraizi kwa mashabiki zangu,”
alisema Tamrina Poshi.
Kwa upande wake, Salma Jabu ‘Nisha’ alisema ndoa ni heshima kwa mwanamke, lakini anachoamini jambo jema hupangwa na Mungu.
“Mungu anatengeneza tutakayerandana na kupendana kiukweli na kuja kudumu
kama wazee wetu walivyokuwa, akimleta hata leo nitaolewa,” alisema.