Story kubwa leo
ni kwamba kuanzia mwakani kila Mwanafunzi wa darasa la kwanza akiripoti
atatakiwa kuja na mche wa mti na ataupanda na kuutunza kwa miaka yote
saba na hatapewa cheti cha kumaliza darasa la saba kabla hajaonyesha mti
wake. Katika shule zenye maeneo madogo, miti hiyo itapandwa katika
maeneo yatakayoelekezwa na Serikali za Vijiji na Mitaa. Kwa wanafunzi wa
Sekondari, itakuwa hivyo hivyo lakini itakuwa miti mitatu.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe January
Makamba amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuanzia mwakani
itatoa maagizo kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa kila
mwanafunzi anayeanza darasa la kwanza katika shule za serikali na zile
za binafsi atahitajika kufika shuleni na mche mmoja wa mti siku ya
kuanza masomo ikiwa kama moja ya mahitaji ya msingi na kwa upande wa
wanafunzi wa sekondari watapaswa kufika na miche mitatu wakati wa kuanza
masomo.
Waziri
Makamba ameainisha kwamba maelekezo yatapelekwa Wizara ya Elimu na
TAMISEMI na moja ya mahitaji ya kupewa cheti cha kuhitimu ni kukabidhi
miti iliyopandwa wakati mwanafunzi anaingia kuanza masomo hivyo
atahitajika kutunza na kuhudumia miti hiyo kipindi chote cha masomo.
Waziri
Makamba ameyasema hayo wakati akishiriki zoezi la upandaji miti na
wanafunzi katika Shule ya Msingi Mlandege iliyopo katika Kata ya
Kwakilosa, Manispaa ya Iringa ambapo aliongozana na viongozi mbalimbali
wa Mkoa wa Iringa. Waziri Makamba ametanabaisha kuwa lengo la kushiriki
zoezi la upandaji miti pamoja na wanafunzi hao ni kutuma ujumbe mahsusi
na wa uhakika kabisa kwamba uhifadhi,usimamizi na utunzaji wa Mazingira
ni jukumu la msingi kwa manufaa ya kizazi kinachokuja na ndio sababu
hasa ya kushiriki na wanafunzi ili waweze kujifunza na kuelewa.
Waziri
Makamba ameainisha kuwa katika shule zenye uhaba wa maeneo yanayoweza
kutumika kwa upandaji miti, maeneo mbadala yatakayoelekezwa na serikali
za vijiji na mitaa.
Waziri
huyo mwenye dhamana ya Mazingira amesema hili linafanyika ikiwa ni moja
kati ya hatua mahsusi, stahiki na za maksudi zinazochukuliwa na
Serikali katika kuendana na mabadiliko ya tabia nchi hasa ikizingatiwa
kuwa asilimia 61 ya nchi yetu ipo katika tishio la kuwa jangwa.
Vilevile
Waziri Makamba amesema kuwa kuanzia tarehe 5-6 Novemba Wakuu wa Wilaya,
Wakurugenzi na Wenyeviti na Mameya wote watakutana Jijini Arusha
Kwaajili ya kupata mafunzo na maelekezo mahsusi yanayohusiana na Hifadhi
ya Mazingira, ikiwemo upandaji miti na utunzaji wa vyanzo vya maji