Monday, December 12, 2016

Kutana na Jambazi mtoto aliefunga mtaa jijini Mwanza na kupora fedha.


Mtoto anayesadikiwa kuwa na umri kati ya miaka 15-17 amefunga Mtaa wa Mecco, Kata ya Nyakato wilayani Nyamagana, Mwanza kwa kupiga risasi hewani na kusababisha taharuki kubwa kwa wafanyabiashara na Wananchi.

Tukio la kijana huyo ‘kufunga mtaa’ limetokea usiku wa tarehe 11Disemba 2016 saa 1:45 katika Mtaa wa Mecco stendi, baada ya (kijana) huyo kutaka kupora katika duka moja linalouza mtungi ya gesi na vifaa vingine.Hata hivyo, katika mapambano ya wawili hao, kijana huyo alianza kupiga kelele zilizosikika, ‘niachieni, niachie’ huku mfannyakazi wa duka hilo akiomba omba msaada kwa watu waliokuwa karibu na duka hilo.

Baada ya watu kufika huku mfanyakazi wa duka hilo, akiita ‘mwizi mwizi,’ watu walifika na kumshika kijana huyo ambapo hata hivyo kijana huyo aliwaponyoka na kutoa silaha iliyokuwa kwenye begi na kupiga risasi moja hewani kuwatawanya watu waliokuwa eneo hilo kutawanyika.

Baada ya kijana huyo kupiga risasi hiyo hewani,gari ndogo nyeupe aina ya 'Saloon' ilifika na kumchukua na kutokomea kusikojulikana na kuwaacha  wananchi wa eneo hilo kupigwa butwaa.

Daud Machota, mmoja wa Wananchi wa eneo hilo amesema kuwa, vitendo vya uhalifu katika eneo hilo vimeanza kutishia amani kwani kumesababisha watu wengi kulala mapema.

“Kwanza mimi ninachoshangaa inakuaje mtoto mdogo wa miaka 15 – 17 anashika silaha na kupiga risasi hewani, labda hawa watoto wanaweza wakawa wamefunzwa mafunzo ya kigaidi, haiwezekani kwa umri wake kufanya hivyo,” amesema Machota.

Machota amesema kuwa, kijana huyo alifanikiwa kuchukua kiasi cha Sh. 40, 000 kwenye duka hilo, huku akidai kwamba uhalifu huo unasababishwa na ugumu wa maisha unaonekana kuwagusa watu wengi.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza na Naibu Kamishna wa Polisi Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akidai kuwa, askari walikuta katika eneo la tukio begi na shati moja.

“Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika uhalifu huo, tunaendelea na uchunguzi kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo, ilipigwa risasi moja hewani,” amesema Msangi.

Chanzo:Mashuhuda wa SHILAWADU,Mwanza.

Comments System

facebook

Disqus Shortname

Powered by Blogger.