TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika siku za hivi karibuni,
kumejitokeza tabia kwa baadhi ya watu wakiwemo wasanii watu wengine
mmoja mmoja kutumia mavazi yanayofanana na sare za Majeshi ya Ulinzi na
usalama hapa nchini likiwemo Jeshi la Polisi katika shughuli zao za
kisanii au katika kazi mbalimbali, Jambo ambalo ni kinyume cha sheria,
kanuni na taratibu za Nchi.
Kwa mujibu wa Sheria ya kanuni za makosa
ya Jinai, sura ya 16 na marejeo yake ya mwaka 2002, kifungu cha 178
(1) na (2) kinachozungumzia makosa dhidi ya sare za majeshi ya ulinzi
na usalama, kinabainisha wazi kuwa ni kosa kisheria kwa mtu yeyote
ambaye siyo mtumishi wa majeshi ya ulinzi na usalama kuvaa mavazi
yanayotumiwa au kushabihiana na sare za majeshi hayo bila kibali kutoka
kwa Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kufuatia kitendo kilichofanywa na kundi
la kisanii la “Original Comedy” kuvaa mavazi yanayoshabihiana na sare
za Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar Es Salaam
linachukua hatua za kisheria dhidi ya wasanii hao.
Aidha Jeshi la Polisi nchini, linatoa
onyo kali kwa mtu ama kikundi chochote kuacha kutumia mavazi
yanayofanana na sare zinazovaliwa na majeshi ya ulinzi na usalama hapa
nchini na atakayebainika hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria
dhidi yake.
Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wale
wote wenye mavazi yanayoshabihiana na sare za majeshi ya ulinzi na
usalama kuzisalimisha mara moja katika vituo vya Polisi vilivyokaribu
nao.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba – Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
Baadhi ya wasanii wa Orijino Komedi wakiwa na MC Pilipili katika harusi ya mwenzao Masanja Mkandamizaji juzi Jumapili.