Kompyuta mpakato zenye majibu ya watu waliopima virusi vya UKIMWI pamoja na majina yao zimeibwa mkoani Tabora.
Kompyuta hizo zipatazo 30 zenye thamani ya TZS 70 milioni, zimeibwa
kwenye ofisi ya shirika lisilo la kiserikali la Jhpiego
linaloshughulika na masuala ya UKIMWI na tohara.
Kompyuta hizo zimeibwa mwishoni mwa wiki kwenye ofisi hiyo iliyo
jirani na ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru). Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Hamis Issa amesema tayari
taarifa za tukio hilo zimewafikia na wanaendelea na uchunguzi wa kina
kufahamu kilichotokea.
Inadaiwa kuwa kompyuta hizo, zina majina ya watu waliopima VVU na majibu yao.
“Kinachotatiza ni kwamba kama majina ya watu wenye virusi
yakijulikana itakuwa ni utata mkubwa kwani ofisi hiyo itakuwa imewaweka
katika wakati mgumu pasipo wao kupenda,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Mkurugenzi wa Jhipego, Dk Albert Komba amethibitisha kutokea kwa wizi huo.
Chanzo: Mwananchi