Sunday, October 9, 2016
Alietaka Mwamunyange apindue nchi aibwaga Serikali Mahakamani.
MWANAFUNZI wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) cha mkoani Arusha, Allan Mbando, ameshinda kesi ya uchochezi ambapo alidaiwa kusambaza ujumbe kupitia Mtandao wa kijamii wa Facebook akimtaka Mwamunyange apindue nchi.
Katika mtandao huo wa kijamii, Mbando, anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka kwamba: “Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje, halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti.”.Aliandika Mbando.
Kutokana na madai hayo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilimfungulia mashtaka Mbando ya kudaiwa kusambaza ujumbe huo uliokusudia kueneza na kufanya uchochezi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo mjini hapa juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Augustine Rwizile, alisema mahakama hiyo imepitia kwa kina hoja na ushahidi wa pande zote mbili katika kesi hiyo.
Hakimu Rwizile alisema baada ya kupitia ushahidi katika kesi hiyo, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo haukuweza kuwasilisha ushahidi unaoweza kumtia hatiani mshtakiwa.
Alisema mbali na ushahidi huo kutojitosheleza, pia hapakuwapo na jambo lolote lenye nia ovu ya kusababisha au kufanya uchochezi katika ujumbe uliosambazwa na mshtakiwa.
“Sasa mahakama hii inamwachia huru mshtakiwa baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka yake pasipo kuacha shaka yoyote....“Lakini pia kama kutakuwa na upande ambao haujaridhika katika hukumu hii unaweza kukata rufaa,” .Alisema Hakimu Rwizile.
Akisoma hukumu hiyo, alisema ujumbe uliosambazwa haukuwa na umuhimu wowote kwa kuwa haukumwelezea Mwamunyange ni nani katika nchi anayotakiwa kuipindua huku pia ujumbe huo ukiwa haukutaja nchi iliyolengwa kupinduliwa.
“Ujumbe ulioandikwa katika Facebook haumtambulishi Mwamunyange ni nani. Lakini ujumbe hauonyeshi jambo la msingi lenye uhusiano wa kisiasa katika Taifa linalodaiwa” .Aliongeza Hakimu Rwizile.
Chanzo;Mtanzania.
Comments System
facebook