Friday, October 14, 2016
Profesa Lipumba atupiwa virago Tanga.
WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, akikamilisha ziara katika mikoa ya Mtwara na Lindi, viongozi wa chama hicho wa Mkoa wa Tanga, hawatampa ushirikiano kama akianza ziara mkoani humo keshokutwa.
Taarifa hiyo imetolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama hicho, Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Jumbe alitoa msimamo huo wakati Profesa Lipumba akitarajiwa kuanza ziara hiyo ya kukiimarisha chama katika Wilaya za Muheza na Korogwe, mkoani hapa.
"Sisi hatutambui ziara hiyo na hatutashiriki kwa sababu yeye si mwenyekiti wa chama chetu kwani alishafukuzwa uanachama na baraza kuu la chama chetu"..."Kwa hiyo, narudia tena hatutashirikiana naye kwa namna yoyote ile, kwa sababu mgogoro aliouanzisha katika chama unaonyesha ni kwa jinsi gani anavyotaka kukidhoofisha chama".Alisema Jumbe.
Hata hivyo aliongeza kuwa viongozi watakaoshiriki katika mapokezi pamoja na ziara hiyo katika wilaya husika, watakuwa wamekiuka miongozo, taratibu pamoja na kununi za chama.
Chanzo:Mtanzania.
Comments System
facebook