KOCHA wa timu ya Real Madrid, Zinedine Zidane, amekiri kuwa anafahamu
ipo siku atatupiwa virago kama hatafikia malengo ya klabu hiyo aliyowahi kuitumikia kama mchezaji.
Kauli hiyo ya Zidane inatokana na mustakabali wa maisha ya kocha huyo
kuwa matatani hasa baada ya timu hiyo kupata matokeo ya sare katika
michezo minne mfululizo ambapo nyota huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa aliiongoza Madrid
kutwaa taji lao la 11 Ligi ya Mabingwa msimu uliopita akiwa kocha wa
timu hiyo kwa mara ya kwanza huku akisisitiza kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa haogopi kutupiwa virago kama kocha wa klabu hiyo tajiri duniani.
“Nafurahia vilivyo kile nikifanyacho. Nina fursa ya kipekee. Naipenda
kazi yangu ambayo si rahisi mara zote, lakini nataka kujifunza kuwa
bora zaidi"...“Najifunza kila siku kufanya kazi na wachezaji bora. Nina kikosi cha
kipekee, iwe tunashinda au kushindwa bado ni wachezaji wema,”.Alisema
Zidane.
Madrid hawajawahi kutoa sare mechi nne mfululizo kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya msimu huu kutokea.
Hata hivyo, kocha wa zamani wa timu hiyo, Fabio Capello, hivi
karibuni alieleza kuwa mwelekeo mbaya wa timu hiyo unasababishwa na
nyota wake, Cristiano Ronaldo ambaye hayupo katika hali nzuri kimwili.
Capello alitoa kauli hiyo na kuongeza kuwa tangu msimu uanze nyota
huyo hayupo katika kiwango kizuri baada ya kupata jeraha la kifundo cha
mguu katika michuano ya Euro 2016 ambayo Ureno ilifanikiwa kuwa mabingwa
wa michuano hiyo.