Wakati watu mbalimbali wakiwa na maoni tofauti kuhusu Chama cha
Mapinduzi (CCM) kupitia Halmashauri Kuu yake kumteua Kanali wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzaia (JWTZ) kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Siasa
na Uhusiano wa Kimataifa, mwenyewe ameibuka na kutolea ufafanuzi uteuzi
huo.
Kanali Ngemela Lubinga (katikati), kulia ni Msaidizi wa Kanali Lubinga, Meja Joseph Masanja na kushoto ni Kapteni Swaleh Omar.
Kanali Ngemela Eslom Lubinga amesema kuwa alishastaafu utumishi wake
jeshini na kuwa angeweza kutumikia chama cha siasa kwani si mtumishi wa
jeshi hilo tena. Kanali Lubinga aliyekuwa Msemaji wa JWTZ alisema kuwa
alistaafu utumishi katika jeshi kuanzia Disemba 2 mwaka huu. Aidha,
alisisitiza kuwa alijiunga na Chama cha Mapinduzi mwaka 1979.
Kikubwa kilichozua maswali kuhusu uteuzi huu ni kwa sababu wanajeshi na
watumishi wengine wa umma hawaruhusiwi kuwa wanachama wa vyama vya
siasa. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waraka wa Utumishi
wa mwaka 2015 unakataza watumishi wa umma kuwa wanachama wa vyama vya
siasa lakini unatambua haki yao ya msingi ya kupiga kura.
Badhi ya maswali yaliyoulizwa na watumiaji wa mitandao ya kijamii ni
lini Kanali Lubinga alijiunga na CCM kiasi cha kuweza kuteuliwa katika
nafasi ya juu kiasi hicho? Kama alijiunga na chama mwaka 1979 inaonyesha
wazi kuwa alikiuka katiba ya nchi inayowataka wanajeshi kutojiunga na
vyama vya siasa.
Akijibu swali hilo Kanali Lubinga alisema kuwa wakati wa mfumo wa chama
kimoja wanajeshi waliruhusiwa kujiunga na chama cha siasa na kuwa baada
ya kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ndipo walizuiwa na kadi
walizokuwa nazo zilichukuliwa.
Kanali Lubinga aliendelea kueleza kuwa kadi zile hazikutupwa bali
zilihifadhiwa na hivyo baada ya kustaafu Disemba 2 mwaka huu akachukua
kadi yake na kuendelea na uanachama wake.
Hata hivyo watu wa kada mbalimbali waliokosoa uteuzi huo wakitaka kuhakikisha kuwa siasa za nchi
haziathiri utendaji wa majeshi yetu na utumishi wa watumishi wengine wa
umma.