WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce
Ndalichako, ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku
akisema Serikali haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa
wapo wa kutosha.
Akizungumza mjini Dodoma jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka
wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), Profesa Ndalichako,
alisema Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo hayo kwa kuwa
inataka kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao idadi yao
ni ndogo.
Pamoja na uamuzi huo mpya, ajira za walimu wapya wa masomo ya
sayansi nazo zimebadilika kwani wale wote waliohitimu ualimu wa sayansi
na hisabati, wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa kituo cha
kazi.
"Kuhusu wale walimu wa ‘arts’, kule tuna walimu wa ziada ambao
tutajaribu kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi walikuwa wamepangwa
shule moja. Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga kulingana na
mahitaji" .alisema Profesa Ndalichako.
Akizungumzia suala la ubora wa elimu nchini, Profesa Ndalichako
aliwataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu kwa
kuwa wao ndio wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.
Chanzo:Mtanzania.