Bingwa wa uzani wa juu wa ndondi
duniani, Mwingereza Tyson Fury amepewa siku 10 na Shirikisho la ngumi za kulipwa Ulimwenguni WBO, kueleza ni kwa
nini asipokonywe mkanda wake wa ubingwa.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 28 Alijiondoa kwenye pambano la marudiano na Wladimir Klitschko wa Ukraine mapema mwezi huu kwa sababu ya matatizo ya kiakili huku akikabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa zisizoruhusiwa,hii ikiwa ni baada ya kukiri kutumia madawa ya kulevya 'coccain' ili kukabiliana na msongo wa mawazo kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga wiki iliyopita.
Tyson Fury (kulia) kwenye pambano lake na Wladmir Klitschko.
Mwenyekiti wa WBO Luis Batista-Salas amesema Fury huenda akapoteza mkanda huo kwa kutoshiriki mapigano, kuvunja mkataba na kwa kutumia dawa zilizoharamishwa kwenye michezo.
Hata hivyo amesema WBO wanajali sana hali yake ya kiafya na wanamtakia afueni ya haraka.
Bondia huyo hajapigana,tangu amshinde Klitschko Novemba mwaka jana.